Chuma cha Reli – Maisha ni movie Lyrics
MAISHA NI MOVIE
Lile la ngombe kula nyasi halafu anatoa maziwa nitakueleza linatokeaje,
Hili la binadamu kula ganda na kutupa ndizi naomba tuliache!
Nawasikitikia waliishi vipi,
Hadi kufikia kutokwa na mvi,
Hawajashtukia maisha yameongezwa chumvi,
Kwa kifupi, ni movie,
Umeona kwa nini nimeliacha lile la kula ganda na kutupa ndizi?
Ni kwa sababu ,kila kitu ni maigizo siku hizi.
Utaelezeaje kinachompelekea mtu timamu kujitia chizi?
Na mwanamke kuamini namuota na nishamweleza sipati usingizi?
Mitaala feki ya elimu,
Binadamu kunywa sumu, eti kisa maisha magumu,
Mapenzi ya mtandao ambayo kwa kawaida hayadumu,
Ni baadhi tu ya maigizo yanayopatikana filamuni humu.
Aki ya nani huu movie lazima utauza.
Hata sioni haja ya kuuchuza
Wenyewe utajiuza,
Wenyewe utajiuza,
Tatizo.
Sijui anayeturekondi alipo,
Tena kwa jinsi hali ilivyo,
Kitakuja kifo kabla ya malipo
Ndugu ,marafiki na jamaa, msinifanye kushangaa,
Kwa kuniambiaa, kinachoendelea sio kazi ya sanaa.